Maungano ya kifalme
Maungano ya kifalme ni hali ya kisiasa na kisheria ambako nchi mbili zinashirikiana mtu yuleyule kama mfalme wao au mkuu wa dola.
Nchi zote mbili zinaendelea kuwa madola ya pekee lakini mfalme ni yeye yule.
Maungano ya aina hii hupatikana katika utaratibu wa utawala wa kifalme lakini haipatikani katika utaratibu wa kijamhuri.
Wakati wa kisasa
[hariri | hariri chanzo]Mifano ni siku hizi hasa Jumuiya ya Madola. Nchi nyingi za jumuiya hii zinamtambua malkia Elizabeth II kama mkuu wa dola kufuatana na katiba ya nchi. Malkia anamteua gavana mkuu kama mwakilishi wake nchini. Katika utaratibu huu nchi hizi zitamtambua pia mfalme au malkia atakayemfuata Elizabeth II kufuatana na sheria za Uingereza kuwa mkuu mpya wa nchi yao.
Nchi ndogo ya Andorra kati ya Ufaransa na Hispania ni mfano wa pekee ambako rais wa jamhuri anakuwa mkuu wa dola wa nchi nyingine. Tangu mwaka 1607 nafasi ya mkuu wa dola wa Andorra hushirikishwa kati ya askofu wa Urgel (Hispania) na mfalme wa Ufaransa. Baada ya mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789 rais wa jamhuri alichukua nafasi ya mfalme wa awali.
Mifano ya kihistoria
[hariri | hariri chanzo]Historia ina mifano mingi ya maungano ya kifalme kati ya nchi mbili zilizoendelea na taratibu zao za pekee lakini kumshirikiana mfalme yeye yule.
- Israel na Yuda zilichanga wafalme Saulo, Daudi na Suleimani kati ya miaka 1025 KK – 926 KK hivi
- Austria na Hungaria zilikuwa na ushirikiano wa kifalme kati ya 1867 na 1918; Kaisari wa Austria alikuwa pia mfalme wa Hungaria.
- Uingereza na Uskoti zilikuwa na maungano ya kifalme kati ya 1603 hadi 1707. Tangu 1707 falme zote mbili ziliunganishwa kuwa "Ufalme wa Britania Kuu" yaani nchi moja.
- vilevile maungano ya kifalme ya Uingereza (tangu 1707 Britania Kuu) na Ueire kati ya 1541 na 1801; tangu 1801 pande zote ziliunganishwa katika "Ufalme wa Maungano ya Britania Kuu na Ueire" hadi 1922.
- Britania Kuu na Ufalme wa Hannover zilikuwa na maungano wa kifalme kati ya 1714 na 1837 ilhali watemi wa Hannover walipokea taji la Uingereza.
- Hispania na Ureno zilikuawa na maungano ya kifalme kati ya 1580–1640
- nchi tatu za Skandinavia yaani Denmark, Uswidi na Norway zilikuwa na maungano ya kifalme chini ya mfalme wa Denmark kati ya 1389–1521; inaitwa pia "Umoja wa Kalmar"